Job 22

Elifazi Anasema: Uovu Wa Ayubu Ni Mkubwa

1 aNdipo Elifazi Mtemani akajibu:
2 b“Je, mwanadamu aweza kuwa wa faida kwa Mungu?
Je, hata mtu mwenye hekima aweza kumfaidi?

3 cJe, Mwenyezi angefurahia nini
kama ungekuwa mwadilifu?
Au je, yeye angepata faida gani
kama njia zako zingekuwa kamilifu?


4 d“Je, ni kwa ajili ya utaua wako ndiyo maana anakukemea
na kuleta mashtaka dhidi yako?

5 eJe, uovu wako si mkuu?
Dhambi zako si hazina mwisho?

6 fUmedai dhamana kwa ndugu zako bila sababu;
umewavua watu nguo zao, ukawaacha uchi.

7 gHukumpa maji aliyechoka,
nawe ulimnyima chakula mwenye njaa,

8 hingawa ulikuwa mtu mwenye uwezo ukimiliki nchi:
mtu uliyeheshimiwa, ukiishi ndani yake.

9 iUmewafukuza wajane mikono mitupu
na kuzivunja nguvu za yatima.

10 jNdiyo sababu mitego imekuzunguka pande zote,
hatari ya ghafula inakutia hofu,

11 kndiyo sababu ni giza sana huwezi kuona,
tena ndiyo sababu mafuriko ya maji yamekufunika.


12 l“Je, Mungu hayuko katika mbingu za juu?
Juu kuliko nyota zilizo juu sana!

13 mHivyo wewe wasema, ‘Mungu anajua nini?’
Je, yeye huhukumu katika giza kama hilo?

14 nMawingu mazito ni pazia lake, hivyo hatuoni sisi
atembeapo juu ya anga la dunia.

15 oJe, utaifuata njia ya zamani,
ambayo watu waovu waliikanyaga?

16 pWaliondolewa kabla ya wakati wao,
misingi yao ikachukuliwa na mafuriko.

17 qWalimwambia Mungu, ‘Tuache sisi!
Huyo Mwenyezi aweza kutufanyia nini?’

18 rLakini ndiye alizijaza nyumba zao na vitu vizuri,
hivyo ninajitenga mbali na mashauri ya waovu.


19 s“Wenye haki wanaona maangamizi yao na kufurahi,
nao wasio na hatia huwadhihaki, wakisema,

20 t‘Hakika adui zetu wameangamizwa,
nao moto umeteketeza mali zao.’


21 u“Mjue sana Mungu ili uwe na amani,
ndipo mema yatakapokujia.

22 vUyapokee mafundisho toka kinywani mwake,
na maneno yake uyaweke moyoni mwako.

23 wKama ukimrudia Mwenyezi, utarudishwa upya:
Kama ukiuondoa uovu uwe mbali na hema lako,

24 xkama dhahabu yako ukiihesabu kama mavumbi,
dhahabu yako ya Ofiri kama miamba ya mabondeni,

25 yndipo Mwenyezi atakuwa dhahabu yako,
naye atakuwa fedha yako iliyo bora.

26 zHakika ndipo utakapojifurahisha kwa Mwenyezi,
nawe utamwinulia Mungu uso wako.

27 aaUtamwomba yeye, naye atakusikia,
nawe utazitimiza nadhiri zako.

28 abUtakusudia jambo nalo litatendeka,
nao mwanga utaangazia njia zako.

29 acWatu watakaposhushwa, nawe ukasema, ‘Wainue!’
ndipo atamwokoa aliyevunjika moyo.

30 adAtamwokoa hata yule ambaye ana hatia,
ataokolewa kwa sababu ya usafi wa mikono yako.”
Copyright information for SwhKC